Nimekuwa nikijiuliza hivi Dunia ingekuwaje kama watu tungekuwa hatuoti? Na je, dunia iko namna gani kwa wale ambao hawana ndoto?
Ni kupitia maswali haya ambako misingi ya maisha yangu yamejengeka. Kwamba, Mungu alikuwa na makusudi makubwa sana na ya kipekee kumuumba mwanadamu na kumpa utashi wa kuota. Kwasababu naamini kuwa dunia bila ndoto, ni sawa na shimo lisilo na uhai, kama ambavyo naamini pia kuwa mwanadamu yeyote yule asiyekuwa na ndoto, basi huyo hana sababu za msingi za ku-justify uwepo wake humu duniani.
Haijalishi nimezaliwa miaka mingapi iliyopita, haijalishi nina umri gani hivi sasa na wala haijalishi kuwa ipo siku nitarejea kwa muumba wangu, jambo pekee ambalo nimekuwa nikiliamini katika maisha yangu ni kwamba, si umri, umbo au wingi wa vyeti ambao utamwezesha mwanadamu kufikia kilele cha mafanikio yake, bali uwezo alio nao katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zimzungukazo. na ndio maana maisha yangu yamekuwa na yataendelea kuwa ya harakati kwani naamini nilizaliwa mpiganani, na naamini nitakufa mpiganaji.
Nikiwa mwanadamu kama ulivyo wewe na yule, ninaamini kabisa kuwa nina mengi sana ya kujifunza toka kwa wanadamu wenzangu kama ambavyo ninaamini pia kuwa kuna mengi ambayo wapo watu wangependa kujifunza kutoka kwangu. Na ndio maana nimeona ni vyema kuanzisha blogi hii ili niwashirikishe wadau wangu wote katika ndoto zangu.
Ninaamini kuwa kupitia blogi hii nitajifunza mengi toka kwenu, na wapo watakaojifunza mengi kutoka kwangu kupitia taarifa zenye kuhusiana na harakati zangu ambazo nitakuwa nikizitoa kupitia blogi hii.
Nina ndoto, naamini nawe una yako, karibu tustawishe ndoto zetu
0 Maoni:
Post a Comment